Ezekiel 8:6-18

6 aNdipo akaniambia, “Mwanadamu, je, unaona yale wanayofanya, haya mambo ya machukizo kabisa nyumba ya Israeli wanayotenda hapa, ambayo yatanifanya niende mbali na mahali pangu patakatifu? Lakini utaona vitu ambavyo vinachukiza zaidi hata kuliko hivi.”

7Kisha akanileta mpaka ingilio la ukumbi. Nikatazama, nami nikaona tundu ukutani. 8Akaniambia, “Mwanadamu, sasa toboa kwenye ukuta huu.” Ndipo nikatoboa ule ukuta, nikaona hapo pana mlango.

9Naye akaniambia, “Ingia ndani, ukaone maovu na machukizo wanayofanya humu.” 10 bHivyo nikaingia ndani na kutazama, nikaona kuta zote zimechorwa kila aina ya vitu vitambaavyo na ya wanyama wachukizao wa kila aina na sanamu zote za nyumba ya Israeli. 11 cMbele yao walisimama wazee sabini wa nyumba ya Israeli, naye Yaazania mwana wa Shafani alikuwa amesimama miongoni mwao. Kila mmoja alikuwa na chetezo mkononi na moshi wa harufu nzuri ya uvumba ulikuwa unapanda juu.

12 dAkaniambia, “Mwanadamu, umeona wanayoyafanya wazee wa nyumba ya Israeli gizani, kila mmoja kwenye sehemu yake mwenyewe ya kufanyia ibada za sanamu yake? Wao husema, ‘Bwana hatuoni, Bwana ameiacha nchi.’ ” 13Akasema tena, “Bado utaona machukizo wanayofanya ambayo ni makubwa kuliko haya.”

14 eNdipo akanileta mpaka ingilio la lango la kaskazini la nyumba ya Bwana, nami nikaona wanawake wameketi hapo, wakimwombolezea Tamuzi. 15Akaniambia, “Unaliona hili, mwanadamu? Utaona vitu ambavyo ni machukizo kuliko hili.”

16 fNdipo akanileta mpaka kwenye ukumbi wa ndani wa nyumba ya Bwana, nako huko katika ingilio la Hekalu, kati ya baraza na madhabahu, walikuwepo wanaume wapatao ishirini na watano. Wakiwa wamelipa kisogo Hekalu la Bwana na kuelekeza nyuso zao upande wa mashariki, wakilisujudia jua huko mashariki.

17 gAkaniambia, “Je, umeona hili mwanadamu? Je, ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda kufanya machukizo wanayoyafanya hapa? Je, ni lazima pia waijaze nchi dhuluma na kuendelea siku zote kunikasirisha? Watazame wanavyonibania pua kana kwamba ninanuka! 18 hKwa hiyo nitashughulika nao kwa hasira, sitawaonea huruma wala kuwaachilia. Wajapopiga makelele masikioni mwangu, sitawasikiliza.”

Copyright information for SwhNEN